Wednesday, June 24, 2015

DARASA LA UFUGAJI

MAZOEA YANAYOWAGHARIMU WAFUGAJI

Kuna baadhi ya wafugaji huwa wanafuga kwa kutegemea uzoefu walionao katika ufugaji bila ya kujali kuwa kuna mabadiliko kila siku katika sekta ya mifugo, wengi wao huwa wanatatua kesi mbalimbali zinazotokea katika ufugaji kwa kutumia uzoefu hali ambayo inawasababishia kupata hasara kubwa isiyo ya lazima. Yafuatayo ni baadhi ya mazoea yanayowagharimu wafugaji:-

1. KUINGIZA VIFARANGA BILA MAANDALIZI SAHIHI
Wengi wa wafugaji huwa wanaingiza vifaranga pasipo kufuata utaratibu wa kitaalam katika kuandaa banda pamoja na maandalizi ya kupokea vifaranga. Na kama atabahatika kufanya usafi basi atafanya juujuu tu hali ambayo inasababisha banda kuhifadhi vimelea vingi vya magonjwa na kupelekea kuku kuugua na kufa kuanzia wanaingia hadi kufikia kuuzwa, na hatimaye mfugaji hupata hasara kwani hutumia pesa nyingi kwenye madawa kwa kutibu na pesa nyingi kwenye chakula kwa kuchelewa kukua kutokana na kuumwa.


2. KULISHA BILA KUFUATA MAELEKEZO SAHIHI
Kila aina ya kuku wanautaratibu wa ulishwaji chakula, utaratibu ambao ukikiukwa huwezi kupata matokeo mazuri ya mifugo yako, ila wafugaji wengi huwa wanalisha kwa utaratibu usio sahihi ambao wao wanadhani kwamba ndio wataongeza uzalishaji wa mayai au watakuwa haraka kwa upande wa kuku wa nyama, na kuna wengine wanadiriki kutumia chakula aina moja mwanzo mwisho, yaan anaweza kutumia chakula cha vifaranga wa nyama (SUPER STARTER) kuanzia mwanzo hadi anauza kuku bila kufaham kwamba kila aina ya chakula ina kazi yake katika kila hatua ya umri. Lakini pia bila kujali kwamba analisha kwa gharama kubwa hali ambayo itampunguzia faida.

3. KUTIBU KWA DAWA AMBAYO SI CHAGUO KWA UGONJWA HUSIKA
Kama inavyofahamika kuwa wafugaji wa kuku wengi wamebarikiwa kwa kufaham majina mengi ya dawa za kuku, na kwa kutumia uzoefu walionao huwa wanatibu kuku wao magonjwa mbalimbali bila kupata maelekezo kutoka kwa Dokta au Mtaalam wa mifugo. Kwa kufanya hivyo hutumia dawa nyingi tofautitofauti kwa kutibu ugonjwa mmoja bila mafanikio na kupelekea ugonjwa kuwa sugu na idadi ya vifo kuongezeka siku hadi siku.

USHAURI: Sio kila mfugaji mzoefu anaweza kuwa Daktari, ila kila Daktari anaweza kuwa mzoefu.



No comments:

Post a Comment