MAFUNZO KWA VITENDO

  SIFA ZA JOGOO NA TETEA BORA

1. SIFA ZA JOGOO BORA

  • Awe na umbo kubwa
  • Awe na ukiko nzuri usioangukia upande mmoja
  • Awe mchangamfu
  • Apende kuwa na himaya yake. Sifa hii utaigundua pindi ukimjazia wapinzani, atakuwa anapigana badala ya kufuata matetea.


2. SIFA ZA TETEA BORA

  • Awe na umbo kubwa
  • Awe na uwezo wa kuatamia
  • Awe na uwezo wa kulea vizuri (high mothering ability)
  • Aweze kutaga mayai ya kutosha.

 



ATHARI ZA KIMAZINGIRA KATIKA ULAJI WA KUKU

Kuna sababu mbalimbali zinazoathiri ulaji wa kuku, athari hizo zinaweza zikamfanya kuku ale sana au asile kabisa. Zifuatazo ni sababu za kimazingira zinazoathiri ulaji wa kuku:-
1. JOTO
Ulaji wa chakula hupungua kadri joto la mazingira linavyoongezeka, kwan kama tujuavyo zoezi la umeng'enyaji wa chakula huongeza joto la mwili, na joto la mwili halitakiwi kupanda wala kupungua, hivyo basi ubongo unamuamuru kuku asile ili kudhibiti joto la mwili lisipande.

Angalizo ni kwamba mfugaji anatakiwa achunge hali ya joto la banda, kwan hata akizidisha balbu au banda likikosa hewa ya kutosha pia inaweza kusababisha joto la mazingira kuongezeka na kupelekea kuku kukosa hamu ya kula hali amabayo itawafanya kuku wadumae.

2. BARIDI
Kipindi cha baridi kuku wanakula sana kwa sababu ubongo unamuamuru kuku ale sana kwa kuwa umeng'enyaji unatakiwa uwe mara kwa mara ili kudhibiti joto la mwili lisishuke.

3. MHEMUKO (STRESS)
Banda likiwa chafu, au lipo sehemu yenye kelele za mara kwa mara, au umeweka kuku wengi katika banda dogo itawasababishia kuku kupata stress hali ambayo itawafanya kuku wakose hamu ya kula.

4. UPATIKANAJI WA MAJI
Maji yanakazi kubwa sana katika umeng'enywaji wa chakula (digestion process), kwa hiyo kuku ukiwabania maji na ulaji wao pia utapungua, kwani zoezi la umeng'enyaji chakula utakuwa unafanyika taratibu sana hali ambayo itawafanya kuku kukaa muda mrefu bila kuhitaji chakula.

5. MUUNDO WA VYOMBO VYA CHAKULA NA MAJI
Muundo mbovu wa vyombo vya chakula na maji utasababisha chakula au maji kuchanganyika na vitu visivyofaa (feed or water contamination) kama vile kinyesi hali ambayo itapunguza ulaji wa kuku.

MADHARA YA KUACHA BANDA CHAFU

Katika ufugaji kitu kikubwa na muhimu kuzingatia ni usafi, bila usafi hata uwe unawapatia chakula aina gani kuku hawawezi kufanya vizuri. Yafuatayo ni madhara yapatikanayo kwa kuacha banda chafu:-

1. MRUNDIKANO WA VIJIDUDU VYA MAGONJWA
Kama tujuavyo banda likiwa chafu kunakuwa na mazalia ya vijidudu vya magonjwa kama vile kuhara damu (coccidiosis), homa ya matumbo (typhoid) na mafua, magonjwa ambayo yanaweza kusababisha vifo vingi katika banda lako na kupelekea kupata hasara.

2. KUKU KUDUMAA NA KUPUNGUZA UTAGAJI
Kuku wakiwa katika ugonjwa wowote dalili ya kwanza kabisa ni kupoteza hamu ya kula hali ambayo inawapelekea kudumaa kwa kukosa lishe bora. Na kwa upande wa kuku wa mayai huwa wanapunguza kutaga au kutotaga kabisa kwa kukosa nguvu ya kuzalishia (production energy).

3. "STRESS " KWA MFUGAJI
Mfugaji anaweza kupata mhemuko (stress) kutokana na kutibu mara kwa mara bila mafanikio kwa magonjwa yaleyale kujirudia, na wingi wa vifo vitavyokuwa vinatokea kila siku.

MAMBO YA KUJIEPUSHA NAYO KATIKA UFUGAJI

Ndugu mfugaji ni ukweli usiopingika wala kujadilika kuwa katika ufugaji kuna baadhi ya mambo wafugaji tunayafanya lakini hayakupaswa kufanyika, yafuatayo ni ya kujiepusha nayo katika ufugaji:-

  • Kuacha banda chafu
  • Kuleta kuingiza kuku wageni bila kujua historia ya chanjo walipotoka.
  • Kuuza kuku wagonjwa.
  • Kuchinja kuku wagonjwa.
  • Kununua kuku wagonjwa.
  • Kutupa kuku waliokufa porini.
  • Kununua chanjo kwa wauzaji wanaofahamika kuwa hawana solar power au jenereta.
  • Kutibu kwa mazoea bila kuwasiliana na Afisa Mifugo.
  • Kutembelea mabanda ya jirani bila kuchukua tahadhari.

ATHARI ZA MINYOO KWA KUKU

Minyoo kwa kuku ina athari nyingi, athari ambazo zinaweza hadi kumpatia hasara mfugaji kama hatozingatia ratiba ya kuwapa dawa ya minyoo kuku wake kila baada ya miezi mitatu. Athari za minyoo kwa kuku ni kama zifuatazo:-
Minyoo mara zote ndani ya mwili wa kuku hutumi virutubisho ambavyo tayari vishameng'enywa na kuku, hali ambayo humfanya kuku kushindwa kurudisha au kufidia nguvu (digestible energy)  aliyoipoteza katika kumeng'enya chakula, atashindwa pia kupata virutubisho vya ukuaji (nutrients  for growth) , na kama haitoshi pia atakosa kupata virutubisho vya uzalishaji (nutrients for production), hali ambayo itamfanya kuku kudhoofika, kudumaa, kupunguza au kutotaga kabisa na hatimaye kufa.

MINYOO (1)

Ipo minyoo ya aina mbalimbali inayoweza kuwapata kuku. Minyoo huenea kupitia maji, chakula na kinyesi.

Dalili za kuku mwenye minyoo
  • Kutoa kinyesi chenye minyoo.
  • Kukosa hamu ya kula.
  • Hudumaa na kukonda (hudhoofika) mwili.
  • Wakati mwingine hukohoa.
Tiba na namna ya kudhibiti minyoo
  • Wapewe dawa haraka baada ya kugundulika kuwa na wanaminyoo, pia wapewe dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu.

GUMBORO (INFECTIOUS BURSAL DISEASE)

Ni ugonjwa wa virusi unaoshambulia na kusababisha vifo zaidi kati ya wiki ya tatu(3) hadi ya sita(6), hushambulia kuku na ndege wengine wafugwao. Ugonjwa huu husababishwa na virusi viitwavyo "BIRNAVIRUS"
Kuenea/kusambaa kwa ugonjwa.
  • Kutoka banda moja kwenda linginge
  • Kupitia kinyesi kinyesi cha kuku anayeumwa
Dalili za Ugonjwa
  • Kuku hutapika na kuharisha majimaji
  • Manyoya husimama
  • Kuku husinzia na kukosa hamu ya kula
  • Vifo hufikia hadi asilimia thelathini (30%)
  • Kuku hujidokoadokoa sehemu ya haja kubwa
  • Cloaca huvimba
  • Chini ya ngozi hasa mapajani vidonda hutokea hasa vifaranga
Namna ya kukinga na kuzuia ugonjwa wa Gumboro
  • Safisha banda kwa dawa za kuua vijidudu (Disinfectants)
  • Wapatie chanjo ya Gumboro vifaranga wakiwa na umri wa wiki 2 na rudia tena wakiwa na umri wa wiki 3 (yaan siku ya 14 na 21)
Tiba za ugonjwa wa Gumboro
Hakuna matibabu ya ugonjwa huu, ila kwa msaada zaidi wasiliana na mtaalam au daktari wa mifugo.

MDONDO/KIDERI (NEWCASTLE DISEASE)

Ni ugonjwa unaowapata jamii ya ndege ambao unasababishwa na vimelea aina ya paramyxovirus.

Kuenea kwa Ugonjwa
Ugonjwa wa Mdondo (Newcastle disease) huenea kupitia njia mbalimbali kama zifuatazo:-

  • Mayai ya kuku aliyeugua ugonjwa wa mdondo/kideri (Newcastle disease).
  • Kugusana na kuku mgonjwa.
  • Kupitia maji yenye maambukizi.
  • Wakati wa totoleshaji vifaranga.
  • Chakula chenye maambukizi.
  • Hewa yenye maambukizi ya ugonjwa huu.



Dalili za Mdondo/Kideri (Newcastle disease)

  1. Vifo vya ghafla.
2. Kutoa udenda mdomoni.
3. Kukosa hamu ya kula.
4. Kuharisha kinyesi cheupe na kijani.
5. Kuhema kwa shida.
6. Kukakamaa viungo au kupooza hasa mabawa, shingo na miguu.


7. Kupunguza utagaji.
8. Vifo hutegemea kasi ya ugonjwa huweza kufikia hadi asilimia mia moja (100%).


Namna ya kudhibiti Mdondo/Kideri (Newcastle disease)


  1. Wapewe chanjo kwa muda unaofaa (Siku ya 7 na 28, na kila baada ya miezi 3).
  2. Kuku wote waliozidiwa (wagonjwa) wachinjwe na wafukiwe katika shimo lenye kina kirefu kuzuia kuenea ugonjwa.
  3. Fuata maelekezo ya Daktari au Mtaalam wa mifugo.
  4. Matibabu
  5. Hakuna matibabu ya ugonjwa huu, ila kwa msaada na ushauri zaidi katika ufugaji wasiliana na Daktari au Mtaalam wa mifugo.

NDUI YA KUKU (FOWL POX)



Ni ugonjwa unaowapata jamii ya ndege, unasababishwa na virusi ambavyo hushambulia katika ngozi (cutaneous form) na katika mfumo wa upumuaji (diphtheritic form).

Njia za kuenea
  • Kugusana na kuku mgonjwa
  • Mbu pia huweza kueneza ugonjwa huu
  • Ndege wa porini
  • Vyombo au vifaa vyenye maambukizo ya ugonjwa
Dalili za Ndui ya Kuku

  • Vidonda kwenye sehemu za wazi kama usoni, miguuni na sehemu ya kutolea kinyesi
 
  • Kupumua kwa shida
  • Macho ya kuku kuonekana kusinzia


Kudhibiti na Kukinga
  • Wapatiwe kinga wakifika umri wa wiki sita(6)
  • Tumia dawa (disinfectant) kusafisha banda kabla na baada ya kutoa kuku
  • Kuku wote wanaougua watengwe au wachinjwe na kufukiwa katika shimo lenye kina kirefu kuepusha muendelezo wa kuwepo kwa ugonjwa wan dui.
Matibabu

Hakuna dawa za moja kwa moja za ugonjwa huu zilizopitishwa kisayansi ila kwa msaada na ushauri zaidi wasiliana na daktari au mtaalam wa mifugo. 

MAHEPE (MARECK'S DISEASE) 

Huu ni ugonjwa unaowapata kuku, ambao unasababishwa na kirusi aina ya "HERPES VIRUS".

Njia za Kuenea au Kusambaa kwa Ugonjwa
  • Kuchanganya mayai yenye ugonjwa na yasiyo na ugonjwa
  • Katika mashine za utotoleshaji vifaranga
  • Mayai ya kuku mwenye ugonjwa huu
Dalili za Ugonjwa wa Mahepe (Mareck's Disease)
  • Kuvimba nerves

  • Miguu na mabawa kuishiwa nguvu (kupooza)
  • Kupungua uzito

  • Sehem ya kuifadhia chakula (crop) kutanuka

  • Macho huharibika na kuwa kipofu (jicho moja au yote)

  • Ngozi huumuka (kuwa nene)

  • Viungo vya ndani huwa na uvimbeuvimbe mweupe

  • Hukosa hamu ya kula

  • Kupooza viungo na vifo hutokea hasa wiki ya 10 hadi 20

  • Kuharisha

Namna ya Kudhibiti na Kukinga
Kuku wapewe chanjo wakiwa na umri wa siku moja (1)

Tiba:
Hakuna matibabu yaliyogundulika kisayansi, ila kama ugonjwa huu umeingia katika mifugo yako wasiliana na daktari au mtaalam wa mifugo aliye karibu yako.

 MAFUA MAKALI (Infectious Coryza)





  Ugonjwa huu huathiri zaidi katika mfumo wa upumuaji na huwapata jamii yote ya ndege.


Njia za Kuenea
Ugonjwa huu huenea zaidi kupitia
         - Hewa
         - Kugusana 
         - Chakula au maji 

Dalili za Mafua Makali


  • Kutokwa na makamasi puani na mdomoni
  • Kupumua kwa shida
  • Kuvimba kuzunguka jicho moja au yote mawili
  • Kupiga chafya
  • Kukosa hamu ya kula
  • Kupunguza uzalishaji (kushusha utagaji au kukua polepole)
Muonekano wa Mapafu Yaliyoathirika na Mafua Makali


Kinga na Tiba ya Mafua Makali
  • Zuia msongamano ndani ya banda
  • Watenge kuku wote wanaougua
  • Wapatie tiba haraka iwezekanavyo kwa kuwapa dawa mojawapo kati ya zifuatazo:-
                   1. Tylo-dox
                   2. Fluban
                   3. Fluquin
                   4. Ganadex
                   5. O.T.C
                   6. Hipraloma

Kwa msaada zaidi wasiliana na daktari au mtaalam wa mifugo aliyekaribu yako.

 HOMA YA MATUMBO (TYPHOID DISEASE)

Ugonjwa huu huwapata jamii yote ya ndege wa nyumbani na wa porini. Ugonjwa huu unasifka kwa kpunguza damu, kuharisha na kupunguza uzito. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria aina ya "Salmonella Gallinarum".

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea

Kupitia maji au chakula chenye maambukizi.
Kugusana kwa wenye vimelea vya magonjwa na kuku wazima.
Kupitia mayai.
Utupaji wa mizoga ovyo.
Wanyama kama paka, mbwa na panya pia wanaweza kusambaza ugonjwa.

Dalili za Homa ya Matumbo (Typhoid)


  • Vifo vya ghafla hutokea.
  • Hupungukiwa hamu ya kula.
  • Hupungukiwa na uzito.
  • Kilemba na mashavu hupauka.
  • Kuwa na homa kali.
  • Kuharisha manjano na hutoa harufu mbaya.
  • Vifo huweza kufikia hadi asilimia thelathini (30%) na zaidi.

Muonekano wa ndani wa kuku mwenye typhoid

Kinga na namna ya kudhibiti Typhoid

  • Tenga kuku wagonjwa.
  • Nyama ya kuku aliyeugua ifukiwe vizuri.
  • USitumie mayai yaliyotagwa na kuku mgonjwa.
  • Kinga na matibabu ya haraka hufaa zaidi.
Matibabu
Typhoid hutibika na hasa kama ikigundulika mapema na kufuata maelekezo ya daktari au mtaalam wa mifugo. Aidha utumie dawa mojawapo kati ya zifuatazo:-
  1. Ganadex
  2. Hipraloma
  3. Typhoprim
  4. Trimazin
  5. C.T.C
  6. O.T.C

KIPINDUPINDU CHA KUKU (FOWL CHOLERA)

 Ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria ambao unaoshambulia karibu aina zote za ndege, ugonjwa huu ni hatari ambapo vifo ni kati ya 30% hadi 80%.

Njia za ueneaji ugonjwa

  • Utupaji ovyo wa mizoga ya kuku, kwani mzoga unaweza kukaa na vimelea kwa zaidi ya miezi mitatu.




  • Kupitia chakula na maji yenye mchanchanyiko na vimelea hivyo.
  • Kuku mzima kugusana na kuku mgonjwa.
  • Kupitia njia ya upumuaji.  

Dalili za Fowl Cholera

  • Huarisha majimaji ya kijani yenye harufu.


  • Kilemba na masikio ya kuku hupauka na kulegea.


  • Hupumua kwa shida.


  • Hutokwa na ute mdomoni na puani.


  • Joto la mwili hupanda.


  • Vifo hutokea  


 Jinsi ya Kudhibiti Fowl Cholera

  • Usafi wa ndani na nje ya banda.
  • Tenganisha kuku kwa rika zao (wakubwa kwa wakubwa na wadogo kwa wadogo).
  • Zingatia sifa za banda bora.
  • Mizoga ichomwe moto au ifukiwe katika shimo la kina kirefu kuzuia kuenea kwa ugongwa.  

Tiba ya Fowl Cholera

Ukiona dalili za ugonjwa huu wahi mapema kutumia dawa mojawapo kati ya zifuatazo:~
  1. Trimazin
  2. Typhoprim
  3. Sulphonamides
  4. Hipraloma
  5. O.T.C
  6. C.T.C 
  7. Ganadex   

SIFA ZA KUKU WENYE AFYA NZURI

1. Huchangamka 








2. Hupenda kula

3. Manyoya hukaa vizuri


4. Pua huwa safi


6. Kuku wa mayai hutaga kwa kiwango kizuri(Si chini ya 80%)

7. Joto la mwili huwa nyuzi joto 42.

8. Hutembea sawasawa bila kuyumba

 

DALILI ZA JUMLA ZA MAGONJWA YA KUKU

1. Kujikunyata

2. Kuzubaa



3. Kushusha mabawa

4. Kudumaa


5. Kukohoa


6. Kukonda

7. Kuharisha

8. Kutoa sauti isiyokuwa ya kawaida(kukoroma)

9. Kuacha kutaga
10.Kupoteza hamu ya kula (anorexia).

 

   KUHARA DAMU KWA KUKU (COCCIDIOSIS)


      Coccidiosis ni ugonjwa wa kuhara damu unaosababishwa na vijidudu wajulikanao kwa jina la "Protozoa". Wadudu hawa hushambulia sehemu mbalimbali za utumbo wa kuku.


Mazingira yanayosababisha coccidiosis. 
  • Unyevu kwenye matandazo/maranda (litter material). 
  • Kutobadilisha matandazo/maranda kwa muda mrefu.

  • Kuhamishia vifaranga kwenye sehemu waliyokuwa wanakaa kuku wakubwa bila kufanya usafi.


Dalili za coccidiosis.
  • Kuharisha; kwanza kinyesi huanza kuwa laini, pili hubadilika rangi kuwa kijivu na baadaye mchanganyiko wa damu na kuonekana kama kahawia au rangi ya udongo au brauni.
 

                                                                
  • Manyoya yasiyo na mpangilio na yaliyosinyaa, kuku hapendezi na hukunja mabawa kama amevaa koti.
  • Kuku kupauka(paleness), hususani kwenye viremba(comb/wattle) na miguuni kutokana na kukosa damu.
  •  Kukua polepole(poor growth).
  •  Kukosa hamu ya kula.

  • Vifo vingi hasa vifaranga.

  • Kupungua uzito.
  • Kushusha utagaji.


 Namna ya kuzuia coccidiosis.
   1.  Epuka unyevu kwenye maranda(litter material) na banda kwa ujumla.  

   2. Tumia dawa za kukinga ugonjwa (coccidiostats).

   3. Badilisha maranda kabla ya kuingiza vifaranga au kuku wapya.


 Jinsi ya kutibu coccidiosis.
Tumia (i)  Esb3 - Kwenye maji au 
           (ii) Amprolium -Kwenye maji. 


MUHIMU
''''''Matibu yote ni muhimu kutumia dawa ya vitamin (multivitamin) kama nyongeza kwa muda wa siku tatu zinazoachana kwa ajili ya kuongeza hamu ya kula''''''





Usikose kufuatilia mfululizo wa mada zetu............................!!!











Imeandaliwa na; 

Dr. Lihundu A. A.
+255 766 828344










8 comments:

  1. Dokta ubarikiwe kwa elim unayotupatia.

    ReplyDelete
  2. asanteni kwa mafunzo mazuri

    ReplyDelete
  3. Ni kweli kabisa dr, kuhusu kushusha mayai hata kuku walipatwa na janga hilo.

    ReplyDelete
  4. Dokta habari, nina kuku wangu wamefikisha wiki nne sasa na ninatarajia kuwauza ila naona vifo vinakuwa vingi, juzi walikufa wawili, jana wawili na leo wamekufa watatu, nini tatizo? Naomba unisaidie dokta.

    ReplyDelete
  5. Pole sana mpendwa, kwanza chunguza mazingira wanayoishi kuku wako kama yapo salaama, pili angalia mazingira unayohifadhia chakula na chakula chenyewe kama kipo vizuri, ukiona vyote vipo sawa muite dokta wa mifugo aje akupe msaada wa kitaalam.

    ReplyDelete