DARASA LA UFUGAJI

LISHE BORA ENDELEVU KWA MATOKEO BORA ZAIDI

Mfugaji ili uwape kuku wako lishe bora yenye kuendelea, na ili upate matokeo bora zaidi katika ufugaji wako wa kuku basi yakupasa kuzingatia yafuatayo:-
  • Tumia chakula bora na siyo bora chakula. Tumia chakula bora ambacho hakina madhara kwa kuku wako na hata walaji kwa ujumla.
  • Weka chakula mahali safi na salama kuepuka wadudu waharibifu kama vile panya ili kuzuia maambukizi ya magonjwa kwa kuku.
  • Tumia kanuni ya "least cost combination" yaan tumia chakula cha bei nafuu kinachotoa matokeo bora zaidi ili kupunguza gharama za ufugaji hali ambayo itakufanya upate faida mara dufu.
Kwa kufanya hivyo utaweza kuwalisha kuku wako chakula kilicho bora kwa matokeo bora zaidi bila kuyumba kiuchumi wakati wote wa ufugaji wako.

KUTUNZA KUMBUKUMBU KATIKA UFUGAJI

Kuna usemi usemao "mali bila daftari hupotea bila habari" ukiwa na mradi wowote wa ufugaji ni vema ukiwa unaweka kumbukumbu za kila siku au kwa kila wiki. Katika kutunza kumbukumbu za ufugaji kuna mambo muhimu ya kuyazingatia kama ifuatavyo:-
1. KUMBUKUMBU ZA KUKU NA UZALISHAJI
Hii ni kuanzia unapowapokea hadi kuwatoa bandani. Hapa unapaswa kila siku uwaangalie kuku wako ili kujua wanahali gani na ni wangapi waliopo, hapo utaelewa kama kuna ugonjwa wa kutibu au tahadhari gani zichukuliwe.
kama ni kuku wa mayai basi kujua idadi ya mayai wanyotaga kila siku, ili uweze kujua asilimia za utagaji na uweze kupima kiwango chao cha utagaji.

2. KUMBUKUMBU ZACHANJO
Weka kumbukumbu za chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile mdondo (Newcastle), gumboro, ndui na magonjwa mengine.

3. KUMBUKUMBU ZA  AFYA
Hapa unarekodi kila aina ya ugonjwa uliotekea bandani, idadi ya walioathirika, waliotibiwa, waliopona na waliokufa. Gharama za matibabu nazo pia ziwekwe kwenye kumbukumbu.

4. GHARAMA ZA VIFAA NA CHAKULA
Vifaa vyote unavyonunua kwa ajili ya ufugaji ni lazima viorodheshwe na viwekwe kwenye kumbukumbu, na gharama za chakula kuanzia unapoingiza kuku hadi unapowatoa iwekwe kwenye kumbukumbu pia.

MUHIMU: Njia rahisi ya kutunza kumbukumbu ni kununua daftari na kutengeneza majedwali yanayoonesha vipengele tajwa hapo juu.

ZINGATIA HAYA ILI UPATE FAIDA ZAIDI

Baada ya kuwa mfugaji amefuata taratibu zote katika ufugaji wake wa kuku kwa lengo la kupata faida, ili mfugaji huyo apate faida zaidi kuna mambo muhimu ya kuzingatia hususan katika kujenga soko lake kama ifuatavyo:-

1. Lenga soko sikukuu za mwisho wa mwaka na zinginezo ambapo kuku huuzwa zaidi.
2. Tafuta masoko ili ujenge jina kwa wanunuzi wakubwa.
3. Jiunge au shirikiana na wenzako kuunda kikundi cha wafugaji (wafuga kuku) ili muweze
  • Kuchanja pamoja kupunguza gharama (kwa wafugaji wadogo)
  • Kutafuta masoko pamoja
  • Kupasiana wateja kama hauna kuku wakati huo
4. Kuweza kujitambulisha katika masoko kwamba Kijiji au kikundi chenu kuku wanapatikana muda wote


FIKIRIA KIKUBWA ANZA NA KIDOGO

Hii ni kwa wote, wafugaji na wanaotaka kuanza kufuga. Unapotaka kuanza ufugaji unatakiwa uanze na ufugaji mdogo hatakama una mtaji mkubwa. Kwa kufanya hivi itakusaidia kupata uzoefu katika nyajna zifuatazo:

1. UTUNZAJI (MANAGEMENT)
Kwa kuanza na kiasi kidogo itakusaidia kujua ni ukubwa gani unafaa kwa kuku wangapi, ukiwa na kuku wangapi utalisha chakula kiasi gani, pia utapata uzoefu wa chanjo muhimu zinazohitajika hali ambayo itakurahisishia pindi utapoanza ufugaji mkubwa.

2. SOKO
Hapa tunalenga upatikanaji wa wateja wa bidhaa zako za mifugo, itakusaidia kujua wateja waliopo wanavutiwa na bidhaa ya aina gani, kwa mfano mayai utajua wanapenda mayai ya kiini cheupe au cha njano? Kwa kufaham wanchokihitaji utajua ufanye nini ili ukidhi wanachokihitaji.

3. CHANGAMOTO
Ukianza na ufugaji mdogo pia itakusaidia kujua changamoto zilizopo kwenye ufugaji na utajifunza ni jinsi gani ya kuzitatua au kukabiliananazo kabla  ya kuanza ufugaji mkubwa.

ULISHAJI WA KUKU WA MAYAI (LAYERS)

Kuku wa mayai ili watage vizuri wanatakiwa walishwe chakula bora kwa utaratibu unaotakiwa, ukiwazidishia au kuwaongezea hawatotaga vizuri. Wanatakiwa walishwe kati na kati kulingana na umri kama ifuatavyo:-

UMRI WA WIKI 1 -2
Katika umri huu wanapewa chakula aina ya "Super Starter" kwa ajili ya kuwatengenezea kinga mbadala ili waweze kuhimili mikiki mikiki ya vijidudu vya magonjwa kadri wanavyoendelea kukua, wanapewa chakula hicho kwa kiwango maalum kama ifuatavyo:-
Wiki ya 1: Gramu 12 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 2: Gramu 22 kwa kuku mmoja kwa siku moja

UMRI WA WIKI 3 - 8
Hapa wanakuwa bado ni vifaranga na wanapewa chakula aina ya "Chick Starter" kwa ajili ya kuendelea kuwajenga miili yao waweze kupoekea virutubisho vizuri, hii inatokana na kwamba kuna baadhi ya viinilishe vinafanya kazi ya kumeng'enya chakula na kupatikana viinilishe vingine, kwahiyo vikikosekana katika mwili wa kuku basi hata wale chakula gani bora, hawawezi kutoa mazao bora, lakini kwa kuwapa "Chick Starter" itawapelekea kuwa na virutubisho hivyo muhimu. Kiwango na ulishaji wake ni kama ifuatavyo:-
Wiki ya 3: Gram 27 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 4: Gram 32 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 5: Gram 38 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 6: Gram 42 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 7: Gram 46 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 8: Gram 50 kwa kuku mmoja kwa siku moja

UMRI WA WIKI 9 - 18
Katika umri huu kuku wanapewa chakula aina ya "Grower Mash" kwa ajili ya kuwakuza na kuwajenga mfumo wa uzazi kwa maandalizi ya utagaji. Kiwango cha chakula kinategemea na wiki kama ifuatavyo:-
Wiki ya   9: Gram 56 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 10: Gram 62 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 11: Gram 64 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 12: Gram 66 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 13: Gram 68 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 14: Gram 74 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 15: Gram 74 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 16: Gram 80 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 17: Gram 82 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 18: Gram 88 kwa kuku mmoja kwa siku moja

UMRI WA WIKI 19 - 40
Huu ni umri ambao kuku wanataga kwa kiwango kikubwa sana (85% hadi 100%) hali ambayo inawafanya kutumia nguvu nyingi mno, hivyo hupewa chakula aina ya "Layers Phase 1" kwa ajili ya kufidia nguvu ya ziada wanayotumia ili waendelee kutaga kwa kiwango hichohicho. Ulishaji wake ni kama ifuatavyo:-
Wiki ya 19: Gram 92 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 20: Gram 102 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 21: Gram 108 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 22: Gram 114 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 23: Gram 116 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 24: Gram 120 kwa kuku mmoja kwa siku moja
Wiki ya 25 - 40: Gram 130  kwa kuku mmoja kwa siku moja

UMRI WA WIKI 41 - 80
Katika umri huu kuku wanakuwa wameanza kuchoka na huanza kutaga kwa kiwango cha kawaida (65% hadi 75%) hivyo hupewa chakula aina ya "Layers Phase 2" kwa ajili kuendeleza (maintain) kiwango chao hicho kwa muda mrefu. Kiwango chao ni "Gram 130 kwa kuku mmoja kwa siku moja".

NB: Kuanzia wiki 81 na kuendelea unaweza kuwauza na kuweka kuku wengine.

MAZOEA YANAYOWAGHARIMU WAFUGAJI

Kuna baadhi ya wafugaji huwa wanafuga kwa kutegemea uzoefu walionao katika ufugaji bila ya kujali kuwa kuna mabadiliko kila siku katika sekta ya mifugo, wengi wao huwa wanatatua kesi mbalimbali zinazotokea katika ufugaji kwa kutumia uzoefu hali ambayo inawasababishia kupata hasara kubwa isiyo ya lazima. Yafuatayo ni baadhi ya mazoea yanayowagharimu wafugaji:-

1. KUINGIZA VIFARANGA BILA MAANDALIZI SAHIHI
Wengi wa wafugaji huwa wanaingiza vifaranga pasipo kufuata utaratibu wa kitaalam katika kuandaa banda pamoja na maandalizi ya kupokea vifaranga. Na kama atabahatika kufanya usafi basi atafanya juujuu tu hali ambayo inasababisha banda kuhifadhi vimelea vingi vya magonjwa na kupelekea kuku kuugua na kufa kuanzia wanaingia hadi kufikia kuuzwa, na hatimaye mfugaji hupata hasara kwani hutumia pesa nyingi kwenye madawa kwa kutibu na pesa nyingi kwenye chakula kwa kuchelewa kukua kutokana na kuumwa.

2. KULISHA BILA KUFUATA MAELEKEZO SAHIHI
Kila aina ya kuku wanautaratibu wa ulishwaji chakula, utaratibu ambao ukikiukwa huwezi kupata matokeo mazuri ya mifugo yako, ila wafugaji wengi huwa wanalisha kwa utaratibu usio sahihi ambao wao wanadhani kwamba ndio wataongeza uzalishaji wa mayai au watakuwa haraka kwa upande wa kuku wa nyama, na kuna wengine wanadiriki kutumia chakula aina moja mwanzo mwisho, yaan anaweza kutumia chakula cha vifaranga wa nyama (SUPER STARTER) kuanzia mwanzo hadi anauza kuku bila kufaham kwamba kila aina ya chakula ina kazi yake katika kila hatua ya umri. Lakini pia bila kujali kwamba analisha kwa gharama kubwa hali ambayo itampunguzia faida.

3. KUTIBU KWA DAWA AMBAYO SI CHAGUO KWA UGONJWA HUSIKA
Kama inavyofahamika kuwa wafugaji wa kuku wengi wamebarikiwa kwa kufaham majina mengi ya dawa za kuku, na kwa kutumia uzoefu walionao huwa wanatibu kuku wao magonjwa mbalimbali bila kupata maelekezo kutoka kwa Dokta au Mtaalam wa mifugo. Kwa kufanya hivyo hutumia dawa nyingi tofautitofauti kwa kutibu ugonjwa mmoja bila mafanikio na kupelekea ugonjwa kuwa sugu na idadi ya vifo kuongezeka siku hadi siku.

USHAURI: Sio kila mfugaji mzoefu anaweza kuwa Daktari, ila kila Daktari anaweza kuwa mzoefu.

MBINU ZA KUKINGA KUKU DHIDI YA MAGONJWA

Tunafahamu kwamba magonjwa ndio chanzo kikubwa cha kukatisha ndoto za mfugaji kutokana na ughali wa bei za dawa au vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo. Lakini upo uwezekano wa kuyaepuka hayo ikiwa tutazingatia yafuatayo kwa uangalifu mkubwa:-
  • Chanja kuku dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyotibika kama vile mdondo, gumboro na ndui.
  • Usifuge kuku na ndege wengine kama vile bata, kanga au kwale katika banda moja. Pia usichannganye kuku wa asili na wa kisasa katika banda moja, yaan kwa mfano usichanganye kuku wa nyama(broilers) na kuku wa asili.
  • Usirudishe nyumbani kuku waliopelekwa sokoni wakakosa soko kwani wanaweza kuleta magonjwa.
  • Ondoa kuku wote wenye dalili za ugonjwa na uwatibu kwa dawa husika, na waliokufa wazike au wachome moto.
  • Watenge kuku wageni kwa takribani wiki mbili kabla ya kuwachanganya na wa zamani.
  • Usafi wa banda, vyombo vya maji na kulishia, na muhudumu ni vya kuzingatia pia.
  • Zuia watu wasiohusika, au ndege kuingia au kukaribia banda.
  • Kuwepo mavazi na viatu maalum vya kuingilia bandani.
  • Mlangoni kuwekwe dawa ya kuulia vijidudu kwa ajili ya kukanyaga kabla ya kuingia bandani.
  • Banda lipumzishwe wiki mbili kabla ya kuingiza kuku wapya.
  • Wape kuku chakula bora na maji safi na salaama. Maji safi na salaama ni yale ambayo hata wewe mfugaji unaweza kuyanywa.

KANUNI ZA  KUONGEZA FAIDA KATIKA UFUGAJI KUKU

Ufugaji kuku ni biashara kama biashara nyingine, kuna wafugaji wengi wanaingia gharama zisizo za lazima katika kufuga kuku hali ambayo inawapelekea kupunguza faida yao na maranyingine hata kutopata faida kabisa, hali hii inawakwaza wafugaji na wengine hukata tamaa kabisa ya kufuga. Lakini hayo yanasababishwa na wao wenyewe wafugaji bila wenyewe kujijua.
Kupitia somo hili tutakumbushana ni namna gani mfugaji anaweza kuzikwepa gharama zisizo za lazima katika ufugaji ili aweze kupata faida mara dufu. Zifuatazo ni kanuni za kuongeza faida katika ufugaji kuku:-

1. KUPATA VIFARANGA BORA
Vifaranga bora ni wale waliototolewa katiaka wakati uliopendekezwa kitaalaam hali ambayo inamjenga kifaranga kuwa na kinga asilia ya mwili ya kutosha, kwahiyo mfugaji anaweza kufuga hadi kufikia kuuza bila kutumia dawa za kutibu ugonjwa wowote zaidi ya chanjo na dawa za kuanzishia tu, hivyo ataokoa pesa nyingi za kumuita daktari na kununua madawa na faida itaongezeka siku hadi siku.

2. ULEAJI MZURI (PROPER MANAGEMENT)
Hapa tunakusudia uasafi wa banda, vyombo vya chakula na maji, maji ya kunywa na muhudumu mwenyewe. Kwan magonjwa mengi ya kuku yanasababishwa na uchafu, hivyo uleaji ukiwa mzuri magonjwa hayatakuwepo halikadhalika na na gharama za matibabu hazitakuwepo pia.

3. CHAKULA BORA
Mfugaji anatakiwa ahakikishe anapata chakula bora kwa ajili ya kuku wake, chakula bora ni ambacho kimekingwa na magonjwa yote na kinakuza kuku kwa wakati, lakin pia chakula bora ni kile ambaho hakisababishi mazingira hatarishi katika banda kama vile kulowesha banda. Chakula ambacho kinalowesha banda kina hatari ya kusababisha magonjwa mbalimbali kama vile coccidiosis na typhoid, hali ambayo mfugaji ataingia gharama za kutibu mara kwa mara na kununua maranda.

4. KUPATA SOKO LA UHAKIKA
Ili upate soko la uhakika ni lazima uwe na tabia ya kutafuta taarifa (search information), kwa kutafuta taarifa itakuwezesha kujua hali ya soko iliyopo ili nawe uweze kujipanga. Na kama ukiwa unategemea tu mtu wa tenga aje mara nyingi utakuwa unalalamikia soko, hali ambayo itakupa stress na kuuza kuku wako kwa bei ya hasara. Ila kama unajua hali halisi ya soko basi hata akija mtu wa tenga nyumbani hatokudanganya na utakuwa na uhakika na bei yako.

FAIDA ZA UFUGAJI KUKU

Tunafaham kuwa unajua faida za kuku lakini ngoja tukumbushe yafuatayo kuhusu faida za ufugaji kuku.
  • Kuku ni chanzo cha haraka cha pesa kwa kuuza kuku au mayai.
  • Kuku wanaweza kabisa kukuongezea kipato na kukuondolea kabisa umaskini.
  • Nyama ya kuku na mayai ni protini muhimu kwa familia, yaan watoto, wagonjwa na hata wazee.
  • Kinyesi cha kuku pia ni mbolea, lakini kama haitoshi maganda ya mayai na manyoya ni mapambo.
  • Hakuna dini wala utamaduni wowote Tanzania unaozuia kula kuku.
  • Katika nyama ambayo haina madhara yoyote katika mwili wa binadamu ni nyama ya kuku na samaki.
  • Ni mradi unaompa fursa kusimamia hata mwajiriwa bila kuathiri ajira yake.
  • Na kwa wale akina fulani katika shughuli za kijadi kuku ni moja ya zawadi au malipo kama mteja hana pesa.

MATATIZO YALETWAYO NA UPUNGUFU WA VITAMINI MWILINI(2)

VITAMINI D
Husaidia madini aina ya calcium na phosphorous kuchukuliwa na mwili ili kuimarisha mifupa na kutengeneza ganda la yai la kuku. Jua husaidia mwili wa kuku kutengeneza vitamini D.

Dalili za Upungufu wa Vitamini D Mwilini

  • Rickets: Mifupa huwa laini(soft), hupinda, magoti huvimba, na midomo huwa laini. Hii hutokana na madini aina ya calcium na phosphorous kutojengeka kwenye mifupa.
  • Maganda ya mayai huwa laini.
  • Kukua polepole.
  • Mayai hupungua.
  • Uanguaji hafifu wa mayai.

VITAMINI E
Dalili za Upungufu wa Vitamini E Mwilini

  • Ugonjwa uitwao "crazy chick" au "nutritional encephalomalacia" ambapo ubongo wa kuku huwa laini na kuathiri mishipa ya fahamu. Dalili zake ni:-
                   -Shingo hupinga
                   -Kifaranga huanguka kifudifudi
                   -Kichaa
  • Majike hupunguza utagaji wa mayai.
  • Mayai hayaanguliwi vizuri

VITAMINI K
Husaidia kuzuia kuvuja damu. Ikikosekana mwilini mishipa ya damu hupasuka na kusababisha damu kuvuja. Vitamini hii hupatikana katika alfalfa, samaki (fish meal) na nyama.

VITAMINI B1 (THIAMIN)
  • Huleta hamu ya kula.
  • Upungufu hufanya kichwa kurudi nyuma (Head retraction)
  •  Siyo rahisi kupata upungufu wa vitamini B1 mwilini kwa kuwa vyakula vingi vina vitamini hii.
  • Hupatikana katika nafaka, alfalfa na mafuta (oil).

MATATIZO YALETWAYO NA UPUNGUFU WA VITAMINI MWILINI(1)


Tofauti na aina nyingine ya vyakula vya kuku, kama vile protini, wanga, mafuta, madini n.k ambavyo vinaweza kutengenezwa mwilini, Ni vitamini K ambayo hutengenezwa katika utumbo wa kuku, na vitamini C hutengenezwa na mwili wa kuku. Vitamini zingine hazitengenezwi mwilini bali ni lazima kuku azipate kutoka kwenye chakula au apewe vitamini zilizotengenezwa viwandani, na zinahitajika katika kiwango kidogo sana mwilini. 
Kuna makundi mawili ya vitamini, nayo ni:-
a/ Vitamini zinazoyeyuka kwenye mafuta (fat soluble vitamins), ambazo ni vitamini A, D, E na K.
b/ Vitamini zinazoyeyuka kwenye maji (water soluble vitamins) ambazo ni vitamini C, B1, B2, B12  na nyingine nyingi.
Kuku huhitaji vitamini zote hizo kwenye chakula, vitamini hizi zote ispokuwa moja (vitamini B12) zikizidi mwilini huondolewa kupitia mkojo. Vitamini B12 inaweza kuhifadhiwa mwilini. Kwa maana hiyo vitamini hizo ni lazima ziwe katika chakula kinacholiwa kila siku (daily diet).
Maelezo haya yanaonesha kuwa kuku anahitaji vitamini 14, kwani vitamini C hutengenezwa mwilini. Ingawa vitamini K nayo hutengenezwa lakini haitoshelezi.
Vitamini C
Husaidia kifaranga kilicho ndani ya yai kukua, mifupa ya kifaranga kuumbika na kukua vizuri, pia mafuta kusambaa vizuri mwilini.

Viatamini A
Huhitajika kwa kiwango kidogo sana katika chakula cha kuku, lakini kiasi hicho kidogo ni muhimu sana kwa kuku ili aweze kukua, kutaga mayai mazuri, mayai yaanguliwe vizuri na macho yaweze kuona vizuri.

Dalili za Upungufu wa vitamini A mwilini.
  • Kuku hukawia kukua.
  • Kuku huwa dhaifu na mwenye manyoya yasiyo na mpangilio.
  • Macho hayaoni vizuri.
  • Utagaji usioridhisha.
  • Mayai yatagwayo hayaanguliwi vizuri.
  • Mayai huwa na doa au madoa madoa ya damu ndani yake (blood spots in eggs)
  • Kukishwa kujikinga na maradhi ipasavyo.
  • Kukonda.
  • Manyoya hayaoti ipasavyo (poor feathering).

UTUNZAJI WA KUKU WANAOTAGA (2)

Dalili au muonekano wa kuku asiyetaga

Kulia kwako ni kuku asiyetaga, na kushoto kwako ni kuku anayetaga
  • Kilemba kidogo, kinaonesha upungufu wa damu na kimesinyaa.
  • Huonekana kama mgonjwa.
  • Miguu yake humeremeta kwa mafuta.
  • Nafasi kati ya nyonga ni ndogo.
  • Nafasi kati ya kifua na nyonga ni ndogo.
  • Tumbo dogo na gumu.
  • Njia ya kutagia (Kenti) ndogo, miringo na imesinyaa.
  • Huita watoto na kuonesha hali ya kutaka kulalia mayai au kulea watoto.

Sababu za kuku kudonoana au kula mayai

  • Lishe mbaya
  • Nafasi ndogo
  • Vyombo havitoshi
  • Kukosa shughuli
  • Mwanga mkali
  • Banda chafu (Manyoya)
  • Ukoo

Namna ya kuzuia kuku kudonoana au kula mayai

  • Kuweka idadi ya kuku inayolingana na sehem ulionayo.
  • Usizidishe mwanga.
  • Banda liwe safi.
  • Weka vyombo vya kutosha.
  • Wape lishe bora.
  • Wape kuku shughuli kwa kuwawekea bembea na sehem ya uwazi kwa ajili ya mazoezi.
  • Kata midomo ya juu.
  • Epuka ukoo wenye tabia hizo.

UTUNZAJI WA KUKU WANAOTAGA (1)


Kuku huanza kutaga wakiwa na umri kuanzia miezi mitano au sita, hii hutegemea aina ya kuku na utunzaji wakati wa ukuaji.

Mahitaji yao


  • Chakula bora cha kuku wanaotaga (layer's mash) gram 120 kwa kuku kwa siku au nusu(1/2) kwa kila kuku wanne kwa siku.
  • Maji - wape maji safi na ya kutosha.
  • Kinga dhidi ya magonjwa kama vile kideri na gumboro kila baada ya miezi mitatu.
  • Usafi wa banda kwa kuondoa buibui, maranda yaliyolowa, kugeuza na kusawazisha maranda kila siku.
  • Usafi wa vyombo vya maji na chakula. Hivi visafishwe kila siku.
  • Kuzuia wadudu kama viroboto na chawa au kuwaangamiza kila wanapoonekana.
  • Kuku wasisongamane; kuku 3 - 4 katika kila meta moja ya mraba.
  • Kuku wapewe majani ya kula ili wasidonoane.
  • Wawekewe viota vya kutosha, kwa wastani wa kiota kimoja cha kutagia kwa kila kuku watano.
  • Kuku wawekewe bembea kwa ajili ya kupumzikia na kulala.

Sababu za kuku kutotaga

Kuku hupunguza utagaji na hata kuacha kutaga kabisa iwapo:-

  • Hawakupewa chakula bora au cha kutosha.
  • Hawapewi maji safi ya kutosha.
  • Wamebanana, yaan hawakai kwa raha.
  • Vyombo vya maji  au chakula havitoshi.
  • Mwanga hautoshi.
  • Majogoo yamezidi (weka jogoo 1 kwa mitetea 10)
  • Kuku wanaumwa.
  • Wana vidusa vya nje na ndani (external and internal parasite).
  • Wamezeeka (umri zaidi ya miaka miwili na nusu).
  • Maumbile ya kuku mwenyewe.

Nini kifanyike


  • Wape kuku chakula bora na cha kutosha (gram 110 - 120 kwa kuku kwa siku).
  • Wape maji safi ya kutosha, wanywe maji saa moja zaidi baada ya kuwalisha chakula.
  • Weka idadi ya kuku inayolingana na nafasi iliyopo. Weka kuku 3 - 4 kwa meta moja mraba.
  • Weka vyombo visafi na vya kutosha.
  • Hakikisha chumba kina mwanga wa kutosha. Mwanga unaowatosha kuku ni ule unaoruhusu mtu kusoma gazeti.
  • Weka idadi ya vyombo kulingana na mitetea iliyopo. Jogoo 1 kwa mitetea 7 - 10.
  • Watenge  na kutibu kuku wagonjwa. Na wachanje kuku ukifuata kalenda.
  • Tibu vidusa vya ndani na nje (external and internal parasite) kwa kufuata ratiba au kila unapoona dalili.
  • Ondoa kuku wazee kwa kuuza au kuchinja.
  • Ondoa kuku wasio taga.

KULEA MITEMBA


Mitemba ni kuku jike wanaokua kuanzia umri wa wiki 9 hadi 20 au hadi wanapoanza kutaga.

Mahali pa kufugiwa
  • Banda bora la kuku lenye sakafu ya maranda au chaga za mbao au waya.
  • Huitaji meta moja ya mraba kwa kuku 5 au 6.
Vyombo vya maji na chakula
  • Huitaji kula na kumywa wakati wote ili wakue na kukomaa, hivyo vyombo vya chakula na maji lazima viwe vya kutosha.
  • Kwa nafasi ya kula, mtemba mmoja huitaji sentimeta 4 kwa vyombo mviringo na sentimeta 9 kwa trough. Na sentimeta 2 nafasi ya kunywa kwa aina zote mbili za vyombo.
Ulishaji
Kuku hawa wanatakiwa kula washibe na kusaza, na chakula chao huitwa chakula cha kukuzia.

Viota
  • Vinatakiwa viwekwe kwenye banda wakati mitemba wanapofika umri wa wiki 16 - 18 ili waanze kuzoea.
  • Viota viwe na ukubwa wa sentimeta 40x30x35 au 30x30x35 kufuatana na utashi wa mfugaji.
  • Kiota kimoja hutumika kwa kuku 4, hivyo kuku 100 watahitaji viota 25.
  • Viota vinaweza kuwa vya chini au vya juu.
Umuhimu wa viota.
  1. Hupunguza kupotea kwa mayai.
  2. Hupunguza kuvunjika kwa mayai.
  3. Huzuia ulaji wa mayai.
  4. Hurahisisha uokotaji wa mayai.
  5. Mayai huwa safi
Bembea (Perches)
Hivi ni vichanja kwa ajili ya kuku kupumzikia wakati wa mchana na kulala wakati wa usiku.
  • Vichanja hivi hutengenezwa kwa kutumia miti na mbao.
  • Kuku wa nyama hawahitaji bembea kwa sababu wao hawawezi kuruka.
  • Kuku wanaokuwa huitaji sentimeta15 za kusimama kwenye bembea na kuku wakubwa huhitaji sentimeta 20 - 30.
  • Vinatakiwa visafishwe angalau mara moja kwa mwezi.
Matunzo mengine ya mitemba
  • Kuondoa kuku wasiofaa, mfano; wagonjwa, waliojeruhiwa, waliodhaifu na wadogo kuliko wastani wa kundi. Shughuli hii huitwa ''culling''.
  • Kutenga na kutibu kuku wagonjwa.
  • Usafi wa banda, nje na ndani. Hii ni pamoja na kugeuza maranda (litters).
  • Kuchanja (vaccination) na kuzuia wadudu kama viroboto nk.
  • Kwa kuku wenye tabia ya kudonoana hukatwa midomo wakati huu.

KULEA VIFARANGA
1.Mahali pa kulelea(Brooder)
   Tayarisha mahali pa kukuzia (brooder) kwa kutumia vifaa vifuatvyo:-
-       Hard board: Kwa ajili ya uzio mviringo, uzio wa eneo la meta moja ya mraba hutosha kulea vifaranga 100 – 150 hadi watakapokuwa na umri wa wiki mbili. Uongezwe kadri vifaranga wanavyoongezeka umri au ukubwa. Uzio uwe na vitundu kwa ajili ya kupitisha hewa.


-       Maranda au nyasi zilizokatwakatwa au magunzi yaliyopondwa kwa ajili ya kufunika sakafu: Hunyonya unyevunyevu na kufanya banda liwe kavu, huleta joto(hutunza joto), hukausha na kuua vijidudu viletavyo magonjwa. Badilisha maranda yaliyolowana.

-        Kileta joto (source of heat): Unaweza infra red bulb, bulb za kawaida, taa ya chemli au jiko la mkaa kwa ajili ya kuleta joto na mwanga. Kileta joto ni vema kiwekwe katikati ya uzio ili pande zote zipate joto la kulingana. Kileta joto kiongezwe au kipunguzwe joto kufuatana na mahitaji ya vifaranga. 
   
Vifuatavyo ni vielelezo vya tabia za vifaranga kwenye brooder endapo:-
i.Joto halitoshi
  Tabia: Vifaranga wanajikusanya karibu na kileta joto.
   Hasara: -  Kukosa hewa kwa sababu ya kulaliana na huwezakufa.
-      Kwa kutokula au kunywa ukuaji huwa ni wa polepole na   
    hatimaye huweza kufa kwa njaa.


  Utatuzi: Ongeza joto kwa utaratibu ufuatao:-
a)     Mkaa – Choma mkaa mwingine na kuongeza kwenye jiko.
b)    Balbu – Ongeza balbu au punguza umbali toka balbu hadi sakafu
             au tumia balbu yenye watts kubwa.
c)     Chemli – Ongeza utambi au ongeza taa.
d)    Uzio – Punguza ukubwa wa mviringo.
e)     Hover – weka hover kuzuia joto lisiende mbali.

ii.Joto kali (Joto limezidi)
   Tabia: Vifaranga wanakimbia kileta joto.

   Hasara: -Vifo hutokea kwa ajili ya joto kali na njaa
                -Kudhoofika kwa sababu ya kutokula
                -Kukua polepole
                -kuota manyoya polepole

 Utatuzi: Punguza joto kwa utaratibu ufuatao:-
             -Mkaa – Punguza mkaa au zima kwa muda
             -Balbu – Punguza idadi ya balbu, tumia balbu ya watts ndogo au
                           ongeza umbali toka balbu hadi sakafu.
              -Chemli – Punguza idadi, pandisha juu au punguza utambi
              -Uzio – Ongeza ukubwa/upana wa uzio
              -Hover – Ondoa hover kabisa

iii.Joto zuri
    Tabia: Vifaranga hula na kunywa kwa furaha, hutawanyika vizuri katika 
                 sehemu zote za brooder.

-         Vyombo vya maji na chakula: Vyombo view bora na visafi, pia vipangwe katika namna ambayo vifaranga wanapata nafasi nzuri ya kula, kunywa na kutembea. Vyombo visafishwe kila wakati maji au chakula kinapobadilishwa.

2. Chakula
    Vifaranga wanatakiwa wapewe chakula bora na salama kwa ajili ya kuchochea ukuaji na kinga dhidi ya magongwa. Chakula kilicholowa na chenye ukungu kisitumike kabisa.

3. Maji
    Maji yasiwe ya joto wala yasiwe machafu, yabadilishwe mara kwa mara na vyombo visavishwe.



Usikose kufuatilia muendelezo wa darasa letu!!!


 

MAANDALIZI YA KUPOKEA VIFARANGA

Brand Poultry Feed
Kwa matokeo bora zaidi, tunajali, tunaelimisha na tunaboresha zaid mifugo yako

Kabla ya kuleta vifaranga

Maranyingi ufugaji wa kuku huanza na vifaranga, na kwa kuwa vifaranga huweza kuathirika haraka na mazingira, maandalizi mazuri kabla hawajaletwa ni muhimu sana.

Vifaranga wakiwa na umri wa juma moja huhitaji eneo la sentimeta za mraba 65 kila mmoja au mete moja ya mraba kwa vifaranga 120 hadi 150.

Kabla hujaingiza vifaranga safisha banda lako vizuri ndani na nje pamoja na mazingira yake. Pakikauka paka chokaa kwenye kuta zote. Hakikisha banda limekuwa tupu kwa wiki moja au mbili baada ya kusafishwa. Tandaza maranda bandani kisha juu yake weka magazeti au "chick papers". 

Hakikisha una idadi ya kutosha ya vyombo vya chakula na maji kulingana na idadi ya kuku. Pia uwe na chakula bora cha kuanzishia.

Tayarisha chanzo cha joto angalau kwa saa 3 - 5 kabla vifaranga havijaingia ili joto la nyuzi joto 33 - 35 lipatikane. 

Ukishawaleta vifaranga
Hesabu na kukagua vifaranga wakati wa kuweka bandani. Changanya maji safi na "glucose" pamoja na dawa za kuanzishia kisha wapatie. Dawa hii wapatie kwa siku 3 hadi 5 kulingana na maelezo ya dawa utakayotumia. Wapatie chakula baada ya saa 2 - 3 toka walipowasili na kunywa maji yenye "glucose" na dawa za kuanzishia.

Tumia kitabu kutunza kumbukumbu ya idadi, tarehe, aina ya vifaranga na chakula, kampuni ya vifaranga, magonjwa na matibabu yake, madawa yaliyotumika na kinga, na vifo toka siku ya mwanzo hadi wakati wa kuuza.

 

SEHEM ZA BANDA BORA LA KUKU

Zifuatazo ni sehem za banda bora la kuku kulingana na aina ya kuku:-

1. Sehem za kutagia (kama ni kuku wa mayai au wa kienyeji).
          Katika banda bora la kuku wanaotarajiwa kutaga inapaswa kuwepo na sehem za kutagia zijulikanazo kwa jina la viota. Viota vinaweza kutengenezwa kwa mtindo wa kuku mmoja mmoja au ushirika.

2. Sehem ya kutembelea.
         Ni ukumbi mkubwa kulingana na idadi ya kuku, ambao ndani yake kunakuwa na vyombo vya maji na chakula, pamoja na kuku wenyewe.

3. Sakafu
         Zipo aina mbalimbali za sakafu kama ifuatavyo:-
    a) Sakafu ya saruji
            Ni vema zaidi ukajenga sakafu ya saruji kisha ukaweka maranda juu yake ili kuzuia ubaridi
         unaotoka sakafuni, na vilevile kupata
wepesi wakati wa kufanya usafi.

     b) Sakafu ya udongo au mawe
             Jaza udongo wa mfinyanzi au mawe kisha siliba vizuri acha pakauke mwisho weka maranda
          kwa wingi.

     c) Sakafu ya chaga
            Banda hujengwa kisha huwekwa chaga umbali wa futi mbili kutoka chini, chaga inaweza
         ikawa ya banzi, "chicken wire" au fito ili kuruhusu kinyesi cha kuku kudondoka choini.

4. Ukuta
         Unaweza kujenga ukuta kwa kutumia nguzo, pamoja na mabanzi au fito kisha kuzibwa vizuri na kuacha sehemu kubwa kwa ajili ya madirisha. Pia unaweza kutumia tofali za kuchoma, saruji au tofali za udongo kwa kujengea na kuacha sehem kubwa kwa ajili ya madirisha.

5. Paa
      Vifaa vya kuezekea vinaweza kuwa ni vigae, nyasi, makuti au bati.


UJENZI WA BANDA BORA LA KUKU 

         Mfugaji anaweza kudhani kuwa mradi wa kuku unaweza kumpatia faida kubwa bila kujali uwepo wa banda zuri na imara.

Banda lililojengwa imara hudhibiti maadui wa kuku na kufanya uzalishaji kuwa bora zaidi.


Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa  ujenzi wa banda.
1. Idadi ya kuku
       Kabla ya kuanza kujenga banda, mfugaji anatakiwa kujua kuwa anataka kufuga kuku wa aina gani na wangapi. Hii itamwezesha mfugaji kujua ukubwa wa banda linalohitajika.


2. Uwezo wa mfugaji kifedha.           Ujenzi wa banda unahitaji fedha nyingi, hivyo ni lazima mfugaji ajue kuwa banda analotaka kujenga atalimaliza.


3. Eneo la kujenga banda.      Mfugaji lazima awe na eneo la kujenga banda na liwe na sifa zifuatazo:-
  • Mwinuko - Iwe sehemu iliyoinuka isiyotuamisha maji kirahisi.
  • Eneo lisiwe mbali na sehemu ya kuishi ili kuweza kulinda.
  • Uwezekano wa upanuzi - Sehemu iwe pana na kubwa ili mradi ukiwa mkubwa iwepo sehemu ya upanuzi.
Sifa za banda bora la kuku.
1. Liwe limejengwa mahali palipokingwa na upepo mkali kwa miti.

2. Liwe na mwanga wa kutosha.

3. Madirisha yaruhusu hewa safi kuingia na chafu kutoka (Cross Ventilation).

4. Sakafu isiruhusu maji kutuama wala maeneo yanayozunguka banda.

5. Paa lisiruhusu mvua kuingia.

6. Banda liwe linasafishika kwa urahisi.

7. Kuta ziwe imara na zizuie wanyama waharibifu kuingia.

8. Banda liwe na nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuku, vyombo vya maji na chakula, na mhudumu
    kupita.






Usikose muendelezo wa darasa letu.......................................!!!!





Imeandaliwa na 


Dr. Lihundu A.A.
+255 766 828344


No comments:

Post a Comment